Ithibati Yatajwa Kuimarisha Uaminifu wa Sekta ya Habari na Uchumi wa Vyombo vya Utangazaji
Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imesema utekelezaji wa mfumo wa ithibati kwa waandishi na watangazaji wa habari nchini ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha uaminifu, weledi na ushindani wa sekta ya habari katika uchumi wa kisasa unaotegemea taarifa sahihi na zenye kuaminika.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji (ABC) uliofanyika Februari 13, 2026 jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema ithibati inalenga kujenga taaluma ya habari yenye misingi imara ya kitaaluma, maadili na uwajibikaji kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.
Ameeleza kuwa mfumo wa ithibati haukusudiwi kudhibiti maudhui ya vyombo vya habari, bali ni utaratibu wa kuweka viwango vinavyolinda hadhi ya taaluma na kuimarisha imani ya umma kwa tasnia ya habari. Amesisitiza kuwa katika mazingira ya sasa ya ushindani wa kidijitali, uaminifu wa chanzo cha habari ndiyo mtaji mkubwa kwa chombo chochote cha habari.
Wakili Kipangula ameongeza kuwa vyombo vya utangazaji vinavyowekeza katika kuimarisha weledi wa rasilimali watu wake vinajiweka katika nafasi bora ya kuvutia wawekezaji, matangazo na ushirikiano wa kimataifa, kwa kuwa soko la habari linazidi kuthamini ubora, uadilifu na uwajibikaji wa kitaaluma.
Kwa upande wa wadau walioshiriki mkutano huo ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeelezwa kuwa ushirikiano kati ya wasimamizi wa maudhui na wadau wa tasnia ni nguzo muhimu katika kujenga sekta imara ya habari inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Hatua ya kuimarisha ithibati inaelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kukuza taaluma za ubunifu na mawasiliano kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa, huku ikihakikisha kuwa sekta ya habari inaendelea kuwa mhimili wa uwazi, uwajibikaji na maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa JAB, waandishi zaidi ya 3,200 kati ya 3,900 walioomba vitambulisho vya uandishi wa habari (Press Card) wamethibitishwa baada ya kukidhi vigezo vya kisheria, hali inayoonesha mwitikio chanya wa wadau na utayari wa sekta ya habari kujiimarisha kitaaluma.