FAQs Contact Staff Mail Feedback Swahili • English

JAB Yampa Onyo Kali Mwandishi kwa Kukituka Maadili ya Uandishi wa Habari

JAB Yampa Onyo Kali Mwandishi kwa Kukituka Maadili ya Uandishi wa Habari
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO BODI YA ITHIBATI YA WAANDISHI WA HABARI (JAB) TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JAB YAMPA ONYO KALI MWANDISHI KWA KUKITUKA MAADILI Dar es Salaam, 23 Februari, 2026 Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa chini ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 na kanuni zake, imempa ONY0 KALI Mwandishi wa Habari, Bw. Kelvin Justine Raphael, mwenye ithibati halali, maarufu kwa jina la ZUNGU (Matejo), kufuatia kukiuka maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika maudhui aliyochapisha kuhusu tukio la uchelewaji wa ndege ya ATCL lililotokea tarehe 21 Februari, 2026. Baada ya kumwita na kumpa fursa ya kusikilizwa kwa mujibu wa taratibu, Bodi imejiridhisha pasipo shaka kuwa mwandishi huyo alitoa kauli zenye matusi, kejeli na lugha isiyo ya staha na isiyozingatia mizania, na misingi ya maadili ya taaluma ya uandishi wa habari. Kauli hizo si tu zimekiuka misingi ya maadili ya uandishi wa habari, bali pia zimeathiri taswira ya taaluma ya habari na kuondoa heshima inayopaswa kuzingatiwa katika utoaji wa taarifa kwa umma. Mwandishi husika amekiri na ameomba radhi kwa makosa hayo. Hata hivyo, Bodi imemtaka kuondoa mara moja maudhui hayo katika majukwaa yote aliyoyachapisha, kuacha mara moja tabia hiyo, na kurejea katika misingi ya maadili, weledi na uwajibikaji wa taaluma yake. Aidha, Bodi inamwonya kuwa endapo atarudia au kuendelea na vitendo vya aina hiyo, haita­sita kuchukua hatua kali zaidi za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kusimamisha au kufuta ithibati yake kwa mujibu wa Kifungu cha 14(b) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023). Bodi inawakumbusha waandishi wote wa habari kuwa uhuru wa kutoa maoni na kuji­eleza hauondoi wajibu wa kuzingatia maadili ya taaluma. Taaluma ya habari ni nguzo muhimu ya jamii inayopaswa kuendeshwa kwa kuzingatia weledi, ukweli, uwiano na matumizi ya lugha yenye staha. Matumizi ya matusi, kejeli na lugha isiyofaa si tu yanadhofisha uaminifu wa mwandishi binafsi, bali pia yanaharibu hadhi na heshima ya taaluma ya habari nchini. IMETOLEWA NA: Patrick Kipangula Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB)