Naibu Waziri Hamis Mwinjuma Aitembelea JAB, Asisitiza Utekelezaji Madhubuti wa Sheria ya Huduma za Habari
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, leo Machi 4, 2026, ametembelea Ofisi za Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) jijini Dar es Salaam ambapo amekutana na watumishi wa Bodi na kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari.
Akizungumza katika kikao na watumishi hao, Mhe. Mwinjuma alisisitiza umuhimu wa Bodi kusimamia utekelezaji wa sheria kikamilifu bila kusita ili kuhakikisha taaluma ya uandishi wa habari inalindwa na kuendelezwa kwa kuzingatia misingi ya weledi na uwajibikaji.
Alieleza kuwa ni muhimu kwa Bodi kuimarisha kanuni na taratibu za usimamizi wa sekta ya habari, pamoja na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaofanya kazi za uandishi wa habari bila kuwa na ithibati rasmi kutoka JAB. Kwa mujibu wake, hatua hizo zitasaidia kulinda hadhi ya taaluma na kuongeza imani ya umma kwa vyombo vya habari nchini.
Mhe. Mwinjuma pia amepongeza juhudi za Bodi katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari tangu kuanzishwa kwake, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuendelea kuimarishwa ili kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa kuzingatia maadili, taaluma na sheria zilizopo.
Katika ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi na kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwa Bodi hiyo.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuanzishwa kwa mifumo ya usajili wa waandishi wa habari, utoaji wa ithibati na vitambulisho vya uandishi wa habari (Press Cards), utoaji wa elimu kwa umma kuhusu majukumu na wajibu wa wanahabari, pamoja na kusimamia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Aidha, Wakili Kipangula alieleza kuwa Bodi imefanikiwa kuandaa na kukamilisha nyaraka muhimu za uanzishwaji wa taasisi chini ya usimamizi wa Msajili wa Hazina, hatua inayoweka msingi imara wa uendeshaji wa taasisi hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu za serikali.
Katika kikao hicho pia zilijadiliwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya habari nchini, ikiwemo uzingatiaji wa maadili katika vyombo vya habari vya mtandaoni pamoja na uhitaji wa rasilimali zaidi ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Bodi.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, pamoja na kuhakikisha kuwa sekta ya habari inaendelea kuimarika kwa kuzingatia misingi ya taaluma, uwajibikaji na maslahi ya umma.